Mwanafunzi wa mwaka wa kwanza, Kitivo cha Sayansi ya Jamii katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Fredrick Joseph (25), ameuawa kwa kushambuliwa kwa kipigo na watu wanaosadikiwa kuwa ni wanafunzi wenzake wakati akitoka klabu ya pombe (Bar).
Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana katika eneo la chuo hicho ambapo mwanafunzi huyo alisikika akipiga kelele ndipo walinzi wakafika na kumkuta akiwa anagalagala njiani. Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, amesema mwanafunzi huyo ambaye ametokea Musoma mkoani Mara alishambuliwa kwa kupigwa sehemu mbalimbali za mwili wake na watu wasiofahamika, katika eneo hilo la chuo hicho huku akisema kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa marehemu huyo alikuwa na ugomvi na watu  katika klabu ya pombe ya Canival Pub iliyopo chuoni hapo na huenda hao ndiyo waliyomvamia na kumpiga.
Walinzi wa chuo hicho waliokuwa doria walimuokota na kumfikisha kwenye kituo kidogo cha polisi kilichopo Chimwaga ambapo alikimbizwa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na ndipo alipofariki wakati akipatiwa matibabu. Kamanda pia amesema hakuna mtuhumiwa hata mmoja anayeshikiliwa na polisi kwa kuwa wote waliomshambulia walitoroka na hawajulikani walipo.