Wasomi na Wanazuoni mbalimbali wamepongeza hatua ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Waziri Mkuu zamani Edward Lowassa kushikana mikono na kusalimiana wakati wa Jubilei ya dhahabu ya miaka 50 ya ndoa ya Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa na Anna Mkapa.
Wanazuoni hao wametoa kauli hiyo leo katika mahojiano maalum na Idara ya Habari iliyokuwa ikitaka kupata maoni yao kuhusu kitendo kilichoonyeshwa na viongozi hao kwa jamii.
Profesa Kitila Mkumbo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amesema kuwa hatua hiyo imeonyesha kuwa huo ndio Utanzania ulivyo wa kutofautiana bila kugombana.
Amesema kuwa kitendo hicho kimewaonyesha wananchi kuwa mazungumzo yana nafasi kubwa ya kuondoa tofauti zilizopo kuliko kutumia njia nyingine kama vile maandamano na mabavu katika kutafuta ufumbuzi wa baadhi ya matatizo.
“Kukutana kwa viongozi hao na kupeana mikono wakati wa kusalimiana kunakumbusha utamaduni wetu uliojingekea toka siku nyingi wa kutatua matatizo yetu kwa mazungumzo bila kugombana au kutumia mabavu,”alisema Profesa Mkumbo.
Kwa upande wa Profesa Joseph Semboja amesema kuwa amefurahishwa sana na kitendo kilichoonyeshwa na viongozi hao kwani kimeuonyesha ulimwengu kuwa Watanzania ni watu wenye Amani na upendo.
Amesema kuwa hatua hiyo imeonyesha kuwa Watanzania wanaweza kuwa na tofauti lakini wakaendelea kuishi pamoja na kushirikiana katika mambo mbalimbali ya kijamii kwa ajili ya maendeleo yao na Taifa lao.
Profesa Semboja amewataka wananchi kujifunza kutokana na kitendo kilichoonyeshwa na viongozi hao ambao wameonyesha kuwa ni lazima wakae pamoja kwa ajili kushughulikia mambo muhimu ya maendeleo ya wananchi badala kuendeleza tofauti ambazo hazina manufaa kwa Watanzania.
Amesema kuwa ipo haja ya kwenda zaidi ya hapo kwa kuweka utaratibu wa kukaa pamoja na kujadiliana ili kutatua vyanzo vya migogoro kwa ajili ya mustakabali mzuri wa Taifa hili.
Profesa amesema kuwa sio sahihi kutumia mfumo wa jino kwa jino kwani utaratibu huo ndio unaoweza kusababisha kukua zaidi kwa migogoro na wakati mwingine unasababisha umaskini kwa wananchi na Taifa kwa ujumla kwani muda mwingi wananchi hawana muda wa kushiriki katika shughuli za maendeleo kwa sababu ya migogoro.
Naye Profesa Samwel Wangwe amesema kuwa hatua ya viongozi hao kukutana na kupeana mikonop ni ishara kwa Watanzania kujifunza kuwa mazungumzo yana nafasi kubwa katika kuleta muafaka mgogoro wowote kuliko kutunishiana misuli.
Amesema kuwa mazungumzo yana nguvu kubwa katika kultea upatanishi katika migogoro mbalimbali inatokea katika jamii kuliko kutumia njia nyingine ambazo zinaweza kusababisha vurugu na uharibifu wa mali za watu na upotevu wa maisha ya watu.
Na Tiganya Vincent, MAELEZO- Dar es salaam