Siku kadhaa baada ya Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu kusikika katika vyobo vya habari akihoji serikali ni sehemu gani ya katiba ya Tanzania inakataza wao kufanya mikutano ya kiasiasa, msemaji wa CCM, Christopher Ole-Sendeka amejitokeza na kutoa ufafanuzi kuhusu jambo hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Ole-Sendeka amesema jambo ambalo Chadema imepanga kulifanya maandamano nchi nzima Sepemba mosi lakini jambo hilo hata kikatiba hawaruhusiwi.
“Katiba ya Tanzania kuanzia ibara ya 12 hadi 28 inatoa uhuru na haki za kila mtu, uhuru wa kujuika, uhuru wa kutoa mawazo, uhuru wa kuabudu vyote vipo humo. Ieleweke kwamba wanachokifanya Chadema ni kuchochea wananchi kwa makusudi kutotii maagizo halali ya vyombo vya dola na serikali kwa visingizo kwamba katika imewapa uhuru huo,
“Katiba haitoi haki na uhuru usio na kikomo. Ibara ya 29 kifungu kidogo cha 5 inasema; Ili watu wote waweze kufaidi haki na uhuru vinavyotajwa na katiba hii kila mtu ana wajibu wa kutenda na kuenesha shughuli zake kwa namna ambayo haitaingilia haki na uhuru wa watu wengine au maslahi ya umma’ sasa wao hayo maandamano hawaoni kama kuna watu wataingiliwa maslahi yao na umma,” alisema Ole-Sendeka.
Aidha aliendelea kusisitiza kuwa pamoja na ibara hiyo kuwabana Chadema kufanya maadamano pia ibara ya 30 kifungu kidogo cha 1 na 2 inaeleza kuwa ni jinsi gani haki na uhuru haviwezi kutumiwa na mtu mmoja kwa ajili ya kuwaathiri wengine.
Pia alisema kuwa wenye sauti ya mwisho kuidhinisha kufanyika kwa mkutano au maandamano ni Jeshi la Polisi na kupitia katiba, ibara ya 11 na kifungu cha 6 na 7, chama cha siasa kinatakiwa kuandika barua Polisi na Polisi wana mamlaka ya kukataa mkutano au maandamano kwa sababu ambazo wataeleza katika maandamano.
Hata hivyo Ole-Sendeka aliwasihi watanzania kuacha kujihusisha na vitendo ambavyo vinaweza kuiingiza nchi katika machafuko ambayo yanaweza kuichafua sifa ya Tanzania kimataifa kwa kufahamika kama nchi kisiwa cha amani.